Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi inautangazaia umma kuwa wahitimu
mahiri 10,629 waliofuzu Vyuo vya Kilimo vya Inyala, Mtwara, Horti
Tengeru, Igurusi, Katrin, Ukiriguru, Maruku, Uyole, KTC Moshi, Mlingano,
Tumbi, Ilonga, NSI Kidatu na Mubondo, wanaweza wakatumiwa kwa lengo
la kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo.
Jumla ya wahitimu 7,525 wamefaulu katika ngazi ya Astashaada
kati ya hao, wanawake ni 2,557 na wanaume ni 4,968. Wahitimu 3,104
wameafaulu katika ngazi ya Stashahada (Diploma) ambapo wanawake ni
774 na wanaume 2,370.
Wahitimu hawa ni mahiri katika michepuo ya Stashahada ya fani
ya kilimo cha mboga matunda na maua (Horticultural Crops), Zana za
Kilimo, Uzalishaji wa Mazao, Umwagiliaji na Huduma za Kiufundi,
Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi ya Kilimo na Chakula na Lishe.
Aidha, Wahitimu hao wanauwezo wa kiutendaji katika kuanzisha
na kutunza bustani za mimea, mboga na matunda, kushauri wakulima kwa
kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo TEHAMA, kusimamia kazi zote
zinazohusu matumizi ya Zana za Kilimo na kuzifanyia matengenezo kila
itapohitajika, kujenga miundombinu ya shamba ikiwemo maghala, vihenge
na mabanda ya wanyama mbalimbali.
Pia wanauwezo wa kuzalisha mazao makuu ya chakula na biashara
yanayolimwa nchini, kusaidia tafiti na kukusanya takwimu za utafiti wa
mazao, kusimamia ujenzi wa miradi midogo ya umwagiliaji na kuandaa
michoro ya miradi hiyo.
Wahitimu hao pia wanao uwezo wa kuandaa mazao baada ya
kuvunwa, kuchakata na kufungasha, kufanya tathmini ya lishe na mahitaji
ya chakula katika jamii, kuandaa mipango na kutoa ushauri kwa jamii
kuhusu masuala ya lishe.
Serikali inawafahamisha Wadau wa maendeleo ya kilimo na
mifugo, Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi na yeyote mwenye
mahitaji yanayoweza kutekelezwa na wataalam hawa kuwa wanayo fursa ya
kuwaajiri, wahitimu hao ili kupata ufanisi katika shughuli zao za
kilimo.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA KILIMO MIFUGO NA UVUVI
18/01/2016
Source: Ministry of Agriculture Food Security and Cooperatives