Mpunga ni miongoni mwa zao muhimu la chakula nchini Tanzania. Uzalishaji wa mchele  nchini kwa takwimu za mwaka 2016 ni zaidi ya tani milioni 2. Tija ya uzalishaji kwa mkulima ni wastani wa tani 1.5 -2.5 wakati katika skimu za umwagiliaji uzalishaji unaweza kufikia hadi tani 6 kwa hekta moja. 
Kilimo kilichozoeleka sana cha mpunga ni kile cha mabondeni ambapo kinahitaji maji mengi. Katika zama hizi za mabadiliko ya tabianchi ambapo kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mvua na maji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji, ni muda muafaka kuanza kuhimiza kilimo kinachotumia maji kwa ufanisi hususan kutumia mbegu za mpunga wa nchi kavu. Aina ya mbegu za mpunga wa nchi kavu ni fursa kwa wakulima wengi zaidi kuzalisha mpunga bila kulazimika kuhitaji maeneo yaliyozoeleka ya mabondeni.
Kilimo mpunga wan chi kavu ni  kilimo gani? Bwana Johnson Tillya ambaye ni Afisa kilimo wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) anasema kuwa, kilimo cha mpunga wan chi kavu ni kile kinacholimwa maeneo yasiyo ya mabonde, na kinachotegemea mvua. Ni kilimo kinachoweza kulimwa sawa na maeneo yanayolimwa mahindi, kwa kifupi ni mpunga wa aina hii hauhitaji maji mengi.

Katika kuhimiza kilimo cha mpunga cha nchi kavu, ASA imeanzisha mashamba darasa kwa ajili ya kutambulisha kilimo cha mpunga wa nchi kavu. Mashamba darasa hayo yalitanguliwa na Mafunzo ya wakulima viongozi pamoja na wataalam wa kilimo yaliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Wakulima cha Mkindo. Wakulima viongozi waliohudhuria mafunzo hayo walipewa malengo ya kuanzisha vikundi vya wakulima katika vijiji walivyotoka ambao watalitakiwa kuwahamasisha kuanzisha mashamba ya vikundi ambayo yatatumika kama mashamba darasa ya kuwafundishia wana kikundi na wakulima wengine. Jukumu jingine la kila mwanakikundi baada ya kupata mafunzo katika shamba darasa ilikuwa ni kueneza elimu waliyoipata kwa angalau wakulima wengine watano.  Kupitia utaratibu huo wakulima wengi zaidi wanaweza kufikiwa kwa kupewa elimu ya kilimo bora cha mpunga wan chi kavu kupitia wakulima wenzao waliokwishapatiwa mafunzo kama hayo awali. Katika mpango huu wa kuhimiza kilimo bora cha mpungu wa nchi kavu, ASA imekuwa na jukumu la kutoa mbegu na Kampuni ya Mbolea Tanzania ilitoa mbolea kwa kila kikundi. 

Mbegu za nchi kavu za mpunga ni zipi? Bwana Tillya alisema mbegu zilizosambazwa kwa wakulima ni NERICA 1, NERICA 2, NERICA 4 na NERICA 7. Sifa za uzaaji wa aina za mpungu wa nchi kavu ni zipi?  Bwana John Teofili, mkulima mwezeshaji wa kijiji cha Tawa alizitaja aina za mbegu za mpunga za nchi kavu na uwezo wake wa kuzaa kama ifuatavyo: NETICA 1 ina uwezo wa kutoa mavuno kilo 1,800 kwa eka, NERICA 2 kilo 1,600 kwa eka, NERICA 4  kilo 2,000 kwa eka, na NERICA 7 kilo 2,000 kwa eka.

Katika ziara ya kutembelea vikundi vya wakulima vinavyoendesha majaribio ya kilimo cha mpunga wa nchi kavu, vijiji vya Kiloka, Tawa, Kisaki na Dala vilitembelewa. Vijiji hivyo vinapatikana Morogoro vijijini katika safu za Milima ya Ulugulu. Msafara huo ulijumuisha Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, Mkoa wa Morogoro, Wakala wa Mbegu za Kilimo na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi. Aidha, Waandishi wa habari wa baadhi ya vyombo vya habari walishiriki ziara hiyo ili kuona mafanikio yaliyopatikana katika kuendesha majaribio ya aina ya mpunga wan chi kavu.
Ziara hiyo ilihitimishwa na Siku ya Wakulima  ya tarehe 1 Juni, 2017 iliyofanyika katika kijiji cha Mtamba, kata ya Mtamba, Tarafa ya Matombo, wilaya ya Morogoro Vijijini.
Source : Wizara Ya Kilimo